VIONGOZI SOKO LA MACHINGA WASIMAMISHWA KUPISHA UCHUNGUZI
VIONGOZI wa soko la wazi la Machinga lililopo Mtaa wa Kitenge, Kata ya Majengo Jijini Dodoma wamesimamishwa uongozi kupisha uchunguzi kutokana na kudaiwa kutenda makosa ya kiuongozi na kijinai kwa wafanyabiashara wa soko hilo.
Amri ya kuwasimamisha viongozi hao imetolewa Septemba 13, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule alipokkwenda kutatua kero za wafanyabiashara wa soko hilo katika Mkutano wa hadhara uliofanyika ndani ya soko hilo.
Mkuu
Katika Mkutano huo Wafanyabiashara walitoa kero zao kwa Mkuu wa Mkoa huku wakirusha kwa viongozi wao ndani ya soko ambao ni Mwenyekiti na Meneja kwa kuuza vizimba kinyume na taratibu pia kughushi barua za Mkurungenzi wa Jiji na vitambulisho vya wajasiriamali.
Mkuu wa Mkoa amesema kuna tuhuma za kiuongozi lakini nyingine za jinai ambazo ni kufoji vitambulisho na barua, hatuna uhakika mpaka uchunguzi ufanyike. Wakati uchunguzi unafanyika Mwenyekiti na Meneja wasimamishwe kwani wameonekana katika sehemu kubwa wao ni tatizo.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Jabir Shekimweri, alisema awali aliunda timu ya uchunguzi ikiongozwa na Kamishna wa TAKUKURU Wilaya kutokana na kero za wafanyabiashara hao alipowasikiliza awali na ilikua na mapendekezo kadhaa ikiwemo kwenye ulipaji ushuru wa siku.
“Kwenye suala la ulipaji ushuru wa soko, Tume ilipendekeza wafanyabiashara wote wasajiliwe kwenye Mfumo na kulipa mara moja au mbili kwa mwezi lakini wapewe control number ya malipo ili yaende moja kwa moja kwenye mfuko wa Serikali na sio mfukoni kwa mtu,” amesema Shekimweri.
Kwa upande wake Mkurungenzi wa Jiji la Dodoma Dk Fredrick Sagamwiko, amesema Ofisi yake ipo mbioni kukamilisha Mfumo mpya wa uendeshaji wa soko ambao unatarajiwa kuanza mapema mwezi Oktoba utakaokwenda kutatua kero zote za wafanyabiashara sokoni hapo lakini kuanzia Septemba 17, 2024, wataanza uhakiki wa kupata idadi kamili ya wafanyabiashara wenye vizimba.
Ujenzi wa Soko la Machinga Jijini Dodoma umegharimu Sh9 bilioni zilizotoka Serikali Kuu na lilijengwa mwaka 2022 kufuatia agizo la Rais wa Tanzania kutaka wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama Machinga wapatiwe eneo maalum la biashara ili kuweka safi Mazingira ya Jiji likiwa na uwezo wa kubeba wafanyabiashara zaidi ya 3,000.
$$$$$$$$$$$