MAKAMU WA RAIS AKUMBUSHIA AHADI KWENYE MAZINGIRA
MAKAMU Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Philip Mpango amesema unahitajika ufadhili unaotabirika, unaoweza kufikiwa endelevu na wenye uwiano kati ya kupunguza na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani.
Dk Mpango ametoa wito huo alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Mkutano wa 35 wa Kamati ya Kudumu ya Fedha ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Makamu huyo amesema nchi zinazoendelea zinahitaji ufadhili zaidi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kufikia azma kuzingatia jinsia katika kwenye ufadhili huo.
Ametoa wito kwa washiriki wa Mkutano huo kufanya mijadala ya kina, kubadilishana uzoefu katika mafanikio, changamoto na mafunzo ili kuweza kupata suluhisho la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na ufadhili unaozingatia jinsia.
Amesema kwa kuunganisha maarifa na utaalamu wa washiriki kutoka mataifa mbalimbali kutawezesha kuongeza juhudi za kitaifa na kimataifa na kuharakisha maendeleo katika kufikia malengo ya pamoja ya ufadhili endelevu wa mabadiliko ya tabianchi unaozingatia jinsia.
Makamu wa Rais amesema mkutano huo unapaswa kusaidia kukumbushia ahadi za nchi zilizoendelea za utoaji wa Dola 100 Milioni kila mwaka ili zitimizwe ifikapo mwaka 2025 ikiwa ni sehemu ya ahadi za nchi hizo za kuwezesha utekelezaji wa mkataba wa Paris.
Kauli mbiu ya Mkutano huo ni kuongeza kasi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia ufadhili unaozingatia jinsia.
Kutokana na kauli mbiu hiyo, amesema Tanzania imeendelea kuhimiza ujumuishaji wa masuala ya jinsia na mabadiliko ya tabianchi kwenye sera, programu na mikakati katika ngazi zote akizitaja sera hizo ni usawa wa kijinsia katika kushiriki shughuli za uchumi, kuweka mazingira rafiki kwa wanawake kushiriki katika uongozi na utoaji maamuzi, usawa wa kijinsia katika elimu, matumizi ya teknolojia pamoja na uwezeshaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia katika maeneo ya mijini na vijijini.
“Jitihada hizo za ujumuishi wa jinsia katika masuala mbalimbali zinalenga kuhakikisha wanawake na wanaume wanapata fursa sawa ya kushiriki, kuchangia na baadae kunufaika na mipango na juhudi za mabadiliko ya tabianchi, ni muhimu tukayazingatia makubaliano haya,” amesema Dk Mpango.
Kwa mujibu wa Dk Mpango, zinafanyika jitihada za kuhakikisha ujumuishaji wa jinsia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hivyo ni muhimu suala la nishati safi ya kupikia kuwa jambo muhimu la kuzingatia katika Mkutano wa 29 wa Mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika mjini Baku nchini Azerbaijan.
Amewambia wajumbe kuwa Tanzania imebeba nishati safi ya kupikia kama ajenda muhimu ya Taifa ambapo lengo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya wananchi wake wawe wanatumia nishati safi ya kupikia kutoka asilimia 7 iliyopo hivi sasa kwani jambo hilo muhimu litasaidia kukabiliana na changamoto za kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi zinazotokana na matumizi ya nishati asilia ya kupikia ikiwemo mkaa na kuni.
$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$