Habel Chidawali-Dodoma
KATIKA Kipindi cha mwaka mmoja (Juni 2023 hadi Juni 2024) jumla ya Polisi 168 wamekutana na adhabu ndani ya Jeshi hilo na wengine wametimuliwa kazi kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo rushwa.
Mbali na Polisi hao, madereva 253 wa magari ya Serikali walikamatwa katika kipindi cha mwaka jana lakini ndani ya miezi sita ya mwaka huu madereva 33 wamefutiwa leseni zao kwa kukosa weledi katika utumishi wao.
Akijibu swali la Makamu wa Rais Dk Philip Mpango kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya Miaka 50 ya Baraza la Usalama wa Barabarani ambaye alitaka kujua hatua zipi zinachukuliwa kwa askari wanaokiuka sheria, Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama wa Barabarani, Deus Sokoni amesema askari 168 walichukuwaliwa hatua ikiwemo kushitakiwa kijeshi na wengine kufutwa kazi.
Katika hotuba yake Makamu wa Rais alisema ajari za Pikipiki zimekuwa zikiongezeka kila mwaka na hivyo Polisi wanatakiwa kusimamia sheria ikiwemo kuwakamata wanaopakia watu zaidi ya mmoja, wasiovaa kofia ngumu na wanaokimbiza mwendo mkali vyombo vyao.
Amesema katika kipindi cha mwaka 2023 jumla ya ajali 435 za pikipiki zilitokea nchini na kati ya hizo, vifo vilikuwa 376 ukilinganisha na mwaka 2022 ambako kulikuwa na vifo 332 jambo alilosema lazima litazamwe na vyombo husika.
Mwenyekiti wa Baraza la Usalama Barabarani ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Daniel Sillo, amesema makosa ya binadamu huchukua sehemu kubwa ya ajari za barabarani lakini Serikali imeandaa mkakati wa kukabiliana na hali hiyo.
Sillo ametaja baadhi ya mikakati hiyo ni kukabiliana na madereva walevi, wanaokimbiza vyombo vya moto kupita kiasi, vyombo visivyo na Bima na wanaoendesha kwa sifa.
&&&&&&&&&&