Mwandishi Wetu – Dodoma
Wadau wa ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara, madaraja, makalavati na majengo nchini wameshauriwa kutumia Maabara za TARURA ambazo zipo katika Mikoa 11 nchini ili kujenga miundombinu yenye ubora
Rai hiyo imetolewa na Fundi Sanifu Mkuu wa Maabara ya TARURA Jacob Manguye wakati akitoa elimu kwa wananchi na mafundi ujenzi waliofika katika Banda la TARURA kwenye maonesho ya Kitaifa ya Nane Nane yanayoendelea Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Manguye amesema kutopeleka sampuli za vifaa vya ujenzi kwenye Maabara husababisha hasara kwa mwenye kazi na kwa serikali lakini kwa wanaofanya uchunguzi kupitia maabala inakuwa nafuu kwao.
TARURA ilianzisha Maabara kwa ajili ya kupima vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kampuni na watu binafsi ikiwemo kazi za barabara zinazo simamiwa na TARURA zinazotekelezwa vijijini na mijini ikiwa na lengo la kusimamia ubora na ufanisi wa miundombinu ya barabara na sekta nyingine za ujenzi”.
Amesema hadi sasa wanazo Maabara kumi na moja (11) zilizosajiliwa na zinafanya kazi kwa ufanisi mkubwa katika mikoa ya Dodoma, Mbeya, Geita, Kigoma, Simiyu, Tanga, Mtwara, Mwanza, Ruvuma, Morogoro na Arusha huku wakijipanga kuifikia mikoa yote nchini.
“Lengo la TARURA ni kuwa na Maabara katika MIKOA yote nchini ili kuweza kupima ubora wa sampuli zinazotumika kujenga miundombinu kama vile udongo, lami au kokoto kutoka kwa wadau wanaotekeleza miradi yao ya ujenzi nchini ili kuwaondolea hasara ambayo wangeweza kuipata,” amesema Manguye.
Kwa upande mwingine Mangunye amewaomba watumiaji wa barabara nchini wakiwemo madereva wa vyombo vya moto kufuata sheria za barabarani kwa kutopitisha magari yenye uzito mkubwa kupita ule unaoruhusiwa kwenye Barabara husika ili kuzilinda barabara zidumu muda mrefu.
Akizungumza na wananchi amewaomba kuacha kufanya shughuli za kibinadamu pembezoni mwa barabara ikiwemo shughuli za kilimo na ufugaji ili kuepusha uharibifu unaweza kutokea kwenye barabara husika ambazo husababisha hasara kwa Serikali.
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&