Na Mwandishi wetu
Kibaha.Katika kipindi ambacho Tanzania inaandaa dira ya Taifa ya maendeleo ya 2025/2050, taasisi zinazosimamia haki madai zimetakiwa kuweka mikakati imara ili malengo makuu yanayotarajiwa yafikiwe bila kikwazo.
Kwa upande wake Tume ya mipango ya Tanzania imeendelea kuratibu na kuandaa dira hiyo kwa njia mbalimbali ikiwemo ushiriki wa wananchi kutoa maoni kwa njia tofauti ikiwemo mitandao ya kijamii na makongamano ya ana kwa ana yanayosimamiwa na wataalamu.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya Mkoa wa Pwani Joyce Mkhoi
Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa wiki ya sheria Kibaha Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Pwani Joyce Mkhoi amesema kutokana na hali hiyo, Serikali imeweka msisitizo kwa taasisi zake kutumia njia mbalimbali ili kufikisha ujumbe kwa wananchi lengo likiwa ni kuongeza chachu na kuijenga jamii kutambua umuhimu wake.
Mkhoi anasema hata kauli mbiu ya mwaka huu juu ya wiki ya sheria inasema Tanzania ya 2050 nafasi ya Taasisi zinazosimamia haki madai katika kufikia malengo makuu ya dira ya taifa, hivyo anaamini kila jambo litakwenda vizuri.
Hakimu huyo amesema kazi kubwa iliyopo kwa taasisi hizo zinazosimamia haki madai ni kujua zimejipangaje hasa katika kutenda haki kwa jamii kubwa ikiwa ni kuzingatia sheria ili kuendelea kujenga taifa lenye amani na utulivu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mawakili wa kujitegemea Mkoa wa Pwani Lita Ntagazwa, amesema kuwa kati ya mawakili 107 wa ndani ya Mkoa huo wameweka kamati ya wanasheria watano ambao wamekuwa wakiwasaidia wananchi wanaokuwa na changamoto za kisheria muda wowote.
“Katika wiki hii tutaendelea kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa jamii na wadau mbalimbali na hatutaishia hapo bali tutaendelea kuzunguka katika maeneo mbalimbali ili kuwafikia wananchi na kuwapa wananchi elimu ya sheria,” amesema.
Mkuu wa mashitaka Mkoa wa Pwani Faraja George amesema kuwa ofisi yao imeendelea kuzingatia matakwa ya serikali juu ya kuweka msukumo wa kuimarisha uundwaji wa dira ya maedneleo ya taifa ya mwaka 2050 hasa kwa kuzingatia haki katika utekelezaji wa majukumu yao kwa jamii.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo ambaye ni katibu Tawala Wilaya ya Kibaha Moses Magogwa amewataka wananchi kuzingatia zaidi njia ya usuruhishi na upatanishi hasa juu ya kesi za madai na si kupambana kwenye ngazi za sheria kwani zinagharama nyingi pamoja na muda.
“Tuzingatie kauli ya usuruhishi hasa kesi za madai maana Serikali inapata hasara kubwa katika maswala ya uchunguzi jamii ingeelewa suala hili ingeweza kuondoa kesi hizo za madai mahkamani na kurejesha kwenye usuruhishi” amesema.
MWISHO