Mwandishi Wetu Bahi
Mvutano mkali kwa pande tatu kati ya Serikali, Mwekezaji na Wananchi umeendelea baada ya kutolewa kwa ekari 27 za Shule ya Msingi Mayamaya katika wilaya ya Bahi kama fidia ya kujengewa Shule ya Sekondari ya kijiji hicho.
Wananchi wa kijiji cha Mayamaya wanapinga kumegwa kwa eneo la shule lenye ukubwa wa ekari 27 na kumpa anayetajwa kuwa mwekezaji ili awajengee shule ya Sekondari wakisema ardhi hiyo ilitolewa kinyemelea na kwamba siyo makubaliano huku wakitaka vyombo vya dola kuingilia kati kuchunguza hata ubora wa majengo yanayojengwa.
Mwishoni mwa wiki wananchi walijikusanya na kwenda kung’oa bikoni zinazotenga mipaka kati ya eneo la shule na hilo linalochukuliwa na mwekezaji ambaye alipitisha katapila na kuharibu mazao waliyokuwa wamelima wanafunzi wa shule hiyo.
Shule ya Msingi Mayamaya iliyopo jirani na Makazi ya Makamu wa Rais Dk Philip Mpango ni miongoni mwa shule chache zenye maeneo makubwa ambayo inakadiriwa kuwa na eneo la ekari 55 walizokuwa wakizitumia wanafunzi katika miradi ya kilimo na walimu wao.
Mwenyakiti wa Kamati ya Shule Iren Mwenda anasema hakuna taarifa sahihi za kuchukuliwa kwa eneo hilo isipokuwa na yeye anashangazwa kuona tajiri mmoja alipoingiza trekta kuharibu karanga na mazao mengine yaliyopandwa na wanafunzi kwa madai wameingia eneo lake jambo alilosema liliwastaajabisha sana.
Mwenda alisema shule haina taarifa za kuchukuliwa kwa eneo hilo na kwamba wasingezuia ujenzi wa Sekondari lakini siyo kujenga kwa kuuza eneo la shule kwa mwekezaji ambaye amechukua upande wa barabarani naye akitajwa kuwa anataka kujenga shule yake binafsi.
“Hivi wapi mliona watu wanafanya mambo kama tuliyofanyiwa sisi watu wa Mayamaya, wanakaa watu wachache wanakubaliana kuuza eneo la taasisi kwa kisingizo cha kujenga shule ya Sekondari wakati kwenye Kata hii tunayo shule na hata madarasa hayajai, kibaya zaidi walifanya figisu wakamhamisha aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa hapa ambaye alikuwa anazuia ndipo wakafanikisha leongo lao,” alisema Mwenda.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa Shule ya Sekondari anasema tangu mwanzo wananchi walishirikishwa na kutoa nguvu zao katika uchimbaji wa msingi na kusogeza mchana ndipo wakaambiwa kuna mfadhiri amejitolea kuijenga shule hiyo lakini bila kushirikishwa kwenye mikutano ya hadhara na hakukuwa na maelezo kwamba mjenzi anachukua eneo la shule kama sehemu ya gharama zake.
Kwa mujibu wa mwakilishi huyo wa wazazi, mbali na wananchi na watu wa mradi wa TASAF, lakini taasisi iliyojulikana kwa jina la ASA walichangia kwenye ujenzi wa shule hiyo ambayo nayo majengo yake yanalalamikiwa kuwa yamejengwa chini ya kiwango na kutengewa kipande ambacho wanafunzi hawatakuwa hata na uwanja wa michezo.
Mwakilishi wa Taasisi ya ASA, Mathias Kanuti alikiri kuwa walichangia kwenye ujenzi huo kiasi kikubwa na kwamba hakukuwa na makubaliano ya namna yoyote ya kupewa ardhi au fedha bali walikuwa wanarudisha sehemu ya faida waliyoipata kwa jamii na tayari walishatambuliwa hata kwa kukabidhiwa vyeti.
Kanuti alisema tangu mwanzo walielezwa uhitaji wa eneo hilo kuwa na shule yao ya Sekondari na kwamba waliokuwa wakijenga ni wananchi wa eneo husika siyo mwekezaji kama inavyoelezwa ndiyo maana hata wao waliamua kutoa mchango wao hapo jambo lililoufurahisha uongozi hata ukawapatia cheti cha kutambua na kuthamini mchango wao.
Alipoulizwa kuhusu mvutano huo, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Bahi Janeth Mayanja aliomba mwandishi kutafuta ufafanuzi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Bahi kwani yeye hakuwa na uelewa wa karibu kuhusu mgogoro huo tangu ilivyokuwa.
Mkurugenzi wa Bahi Zainabu Mlawa alikiri kuufahamu mgogoro huo lakini akasema mwekezaji huyo alipewa kihalali eneo hilo la shule kwenye mkutano wa hadhara ili awajengee wananchi shule ya Sekondari na baadae kuikabidhi kwa serikali jambo alilosema linaendelea kutekelezwa hadi sasa.
Kuhusu taratibu za utoaji wa maeneo ya umma ikiwemo shule kwamba zinatakiwa kupitia njia zipi, alisema bado anafuatilia kama kulikuwa na ukiukwaji isipokuwa hadi wakati huu anachotambua yeye ni mwendelezo wa ujenzi wa shule ya Sekondari kama fidia ya mhusika ambaye hakumtaja jina lake ili alichukukue eneo la shule ambalo walikubaliana na viongozi wa Kijiji kwa wakati huo.
@@@@@@@@@@@@@@@@@