Habel Chidawali-Dodoma
KANISA la Anglikana Tanzania limeiomba Serikali kuwazuia viongozi wa dini wanaoanzisha makanisa mapya kuacha kutumia majina ya zamani kwani inapelekea baadhi ya waumini kuwa watumwa wa Imani.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne na Katibu Mkuu wa Anglikana Tanzania Mchungaji Canon Bethuel Mlula ambaye amesema kumeibuka mtindo wa baadhi ya watu kutumia majina yanayoshabihiana na makanisa ya zamani ili kupoata usajili jambo alilosema linavuruga Amani.
Wito wa Mchungaji Mlula umekuja baada ya mgogoro wa kanisa hilo na kanisa jipya la Episcopal Anglikana Church katika Dayosisi ya Mpwapwa uliotokana na aliyekuwa mgombea nafasi ya Uaskofu Elibariki Kuta ambaye jina lake liliondolewa kwa kukosa sifa walipobaini kuwa mke wake wa zamani walitengana.
Kiongozi huyo ameiomba Serikali kuwata viongozi wa dini kuacha mara moja tabia hiyo na kwamba mamlaka za usajili zinapaswa kulitazamani jambo hilo haraka iwezekanavyo.
“Tunaiomba Serikali kuingilia kati jambo hili, hawa watu wanaoanzisha makanisa mapya wamekuwa na mtindo wa kutumia majina yanayoshabihiana na makanisa ya zamani kwa lengo la kupata waumini na hili siyo sahihi,” amesema Mlula.
Akimzungumzia Kuta, amesema ni mtu aliyekosa sifa kwa mujibu wa Katiba ya Kanisa hilo ikiwemo kuishi na mwanamke mwingine wakati mke wa kwanza yupo, kushindwa kwenda mbele ya Askofu wake na kula kiapo cha utii na kuwakashifu viongozi wa Kanisa hilo ikiwemo Maaskofu kwa kuwaita mafarao.
Mchungaji Canon Mlula amemwomba Kuta na wachungaji waliohama Kanisa hilo kuacha kutumia mali za kanisa na kubadiri mavazi ili kuepusha mgogoro na mgongano baina yao.
Kwa mujibu wa Mchungaji Mlula, baada ya kukosa sifa za kugombea Cheo cha Askofu Dayosisi ya Mpwapwa, alihamasisha baadhi ya wachungaji kujiunga naye ambao waliondoka na waumini karibu makanisa saba.
Migogoro ndani ya Kanisa hilo ilianza mwanzoni mwa miaka 2000 lakini mgogoro mkubwa ulishuhudiwa kati ya aliyekuwa Askofu wa Kanisa hilo Dayosisi ya Central Tanganyika Marehemu Godfrey Mhogolo na aliyekuwa msaidizi wake Askofu Ainea Kusenha ambapo Kusenha alianza Kanisa lake lakini halikupata usajili.
@@@@@@