Habel Chidawali-Bahi
KADA ya walimu imetajwa kuwa muhimu zaidi katika kuliandaa Taifa licha ya ukweli kuwa watumishi kwenye sekta hiyo wamekuwa wakidharauliwa mara nyingi.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Bahi Rebeka Nsemwa, wakati akizungumza na wazazi na wanafunzi katika shule ya Sekondari ya Mpinga alipokuwa akipokea madawati, viti na meza vuilivyotolewa na Benki ya NMB kwa shule kadhaa wilaya kwake.
Nsemwa alisema kazi kubwa inayofanywa na walimu inastahili heshima na kutokupuuzwa kwani hakuna mafanikio yanayopatikana popote kama walimu hawakujenga msingi mzuri vichwani mwa watu.
Mkuu huyo aliwaomba Walimu kufanya kazi kwa kujituma zaidi na kupokea kila jaribu lakini watambue kuwa utumishi wao unahesabiwa hata mbele za Mungu hivyo watalipwa kadri inavyowaapswa.
Aliwaagiza walimu kuongeza nidhamu na utii kwa walimu wao na kuwaheshimu mahali popote wanapokutana nao hata watakapomaliza masomo yao yao kuanzia hadi elimu ya vyuo vikuu.
“Hata mimi nilikuwa shuleni kama ninyi tena miaka siyo mingi iliyopita, naomba sana muwaheshimu walimu hawa, jamani sisi tuliofika huku tuliko tunajua mchango mkubwa walimu wetu kwamba bila wao tusingefika hapa tulipo, nawasihi sana wanangu na wadogo zangu wapeni heshima walimu,” alisema Nsemwa.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo aliagiza kutolewa kwa motisha ya walimu wanaofanya vizuri ikiwemo wenye usimamizi mzuri wa kitaaluma na kufaulisha watoto akisema kuwa ataanzisha jambo hilo yeye mwenyewe mara baada ya matokeo ya mwaka huu.
Mbunge wa Bahi Kenneth Nolo aliahidi kuunga mkono suala la kutoa motisha kwa walimu ndani ya wilaya hiyo akisema litasaidia kuiweka kilele wilaya hiyo ambayo imeongeza ufaulu zaidi hata huingia kwenye wilaya 10 bora Kitaifa huku ikishika nafasi ya kwanza mkoa wa Dodoma.
@@@@@@@@@@