WAZIRI CHANA, DKT. ABBASI WAKUTANA NA MACHIFU, SONGEA
MACHIFU nchini wamepongezwa kwa kazi kubwa wanazofanya kwa kushirikiana na Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan katika Kuimarisha amani na Utulivu nchini jambo linalotajwa kuleta utulivu.
Pongezi hizo zimetolewa leo Septemba 22,2024 na Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi, Dk Pindi Chana (Mb) aliyeambatana na Katibu Mkuu, Dk Hassan Abbasi Mkoani Ruvuma walipokutana na Machifu kutoka makabila mbalimbali ya hapa nchini kwenye ziara ya kutembelea Makumbusho ya Historia ya Vita vya MajiMaji Mjini Songea.
Ziara hiyo ni sehemu ya Maandalizi ya mapokezi ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan anayetarajiwa kuitembelea Makumbusho hiyo ambayo ni moja ya maeneo yenye historia kubwa hapa nchini.
Balozi Dk Chana aliwahakikishia Machifu kuwa Wizara anayoingoza itaendelea kushirikiana nao katika Uhifadhi na kuendeleza urithi wa Kihistoria nchini ili Watanzania waweze kunufaika na Mazao hayo ya Utalii wa Historia na Malikale.
Mbali na kukutana na Machifu hao, Balozi Chana amekagua maandalizi ya mapokezi ya Rais Samia kwenye Makumbusho hiyo iliyohifadhi Historia adhimu na adimu katika ukombozi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla dhidi ya Ukoloni Miaka takribani 119 iliyopita.
Kwa mujibu wa Waziri, kila kitu kwenye maandalizi hayo kimekaa vizuri na hivyo anayesubiriwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye naye ni Chifu ili ashiriki kwenye kumbukizi hiyo akiwa na machifu wengine na viongozi wa Serikali.
$$$$$$$$$$