”MKOA WA TABORA WAPANGA MKAKATI KUWAKABILI VISHOKA WA UMEME
SERIKALI Mkoani Tabora imewaagiza mafundi umeme wote wanaotambuliwa kuhakikisha wanakuwa na leseni za kuwatambulisha ambazo zinatolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa mujibu wa kifungu namba 8 (h) cha sheria ya umeme sura 131 ili kuepuka usumbufu.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dk John Mboya, wakati akifungua semina ya siku moja kwa mafundi umeme wa mkoa huo alipokwenda kumwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora,Paul Matiko Chacha.
Dk Mboya amesema kuanzia Septemba 17,2024 Mkoa wa Tabora umepiga vita mafundi vishoka, akisema kuwa anaamini baada ya Serikali hiyo kila fundi asiye na leseni ataomba ili afanye kazi kwa uhalali huku akiwasihi mafundi kutokupoteza fursa muhimu waliyopatiwa.
“Ninawasihi sana tusipoteze fursa hii kwani mkoa wetu una miradi mingi ambayo ni fursa kwa mafundi umeme na kuanzia sasa vishoka wote hawatapewa kazi mpaka pale watakapokuwa na leseni ya EWURA, hili ni takwa la sheria ambalo lazima tulifuate,” alisema Dk Mboya.
Meneja wa EWURA Kanda ya Magharibi, Mhandisi Walter Christopher, alisema semina hiyo iliyowashirikisha mafundi umeme na wadau zaidi ya 150, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wataalam na wadau hao kuhusu sheria, kanuni, miongozo na utaratibu wa utendaji kwenye shughuli za ufungaji wa mifumo ya umeme.
Wadau wengine walioshiriki semina hiyo ni Wakala wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Wakala wa Majengo (TBA) na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA).
Kwa mujibu wa Ewura, mafundi umeme wanaweza kuomba leseni kupitia mfumo wa LOIS unaopatikana kwenye tovuti ya EWURA www.ewura. go.tz na kupakua fomu ya kukamilisha ufungaji mifumo ya umeme katika tovuti hiyo hiyo au kuwasiliana na EWURA kwa simu 0800110030, mitandao ya kijamii au barua pepe; info@ewura.go.tz.
&&&&&&&&&&&WhatsApp Unknown 2024-09-18 at 14.03.32