Habel Chidawali-Dodoma
UCHAGUZI wa Serikali za Mitaa umepengwa kufanyika Novemba 27,2024 hapa Tanzania huku vyama vyenye usajili wa kudumu vikiwa na taarifa sahihi za kalenda nzima ya uchaguzi huo.
Kipenga cha uchaguzi kilishapulizwa na Waziri mwenye dhamana kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi Mohamed Mchengerwa ambaye pia alitangaza ukomo wa viongozi kwa nafasi hizo kwamba itakuwa Oktoba 25,2024.
Watu 59,851,347 wa Tanzani Bara (sensa ya watu na makazi NBS-2022) watakuwa kwenye mchakamcha wa kusaka viongozi hao ambapo Mjini jumla ya watu 20,618,348 miongoni mwao watapatikana viongozi wa Mitaa huku watu Vijijini watu 39,232,999 nao watapata viongozi wa Vijiji,Vitongoji na wajumbe.
Watanzania watafanya uchaguzi huu katika nafasi za Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa,Vitongoji na wajumbe watakaounda Halmashauri za Vijiji na Serikali za Mitaa.
Huu ni uchaguzi muhimu kuliko uchaguzi wa mwakani hasa kwa chama chenye malengo ya kuunda dola kwani huu ndiyo msingi imara kwa mjenzi wa nyumba.
Huwezi kupaka rangi nyumba iliyojengwa msingi mbovu halafu ukatangazia watu kwamba una jengo zuri kumbe ni rangi ya juu chini msingi na kuta haviko imara.
Tunashuhudia baadhi ya vyama vikifanya maandalizi ya kusaka wapiga kura, vingine bado vinatafuta namna uchaguzi utakavyoendeshwa hasa kwa usimamizi ndiyo maana wamekimbilia mahakamani kwa lengo la kutafuta tafsiri za kisheria.
Mbali na makundi hayo, kuna vyama havijui kuwa uchaguzi ni kama chungu cha moto kilichowekwa juu ya jiko la moto huku ndani yake kukiwa chakula na wao wananjaa lakini wakisubiri mlo wa huruma. Haiwezi kutokea.
Waliokwenda mahakamani wanajipanga kuwa na wagombea, wanaohangaika mtaa kwa mtaa kutoa hamasa na kuwafunda makada wao mbinu za kuwapata wagombea na wapiga kura nao wamejindaa, je walionyamaza wanakuja kwa gia ipi.
Inawezekana ukimya wao ni moja ya mbinu za kuwadanganya adui wasijue njia wanazopita, lakini ukweli ni kuwa mojawapo ya mbinu kwenye uchaguzi huwa ni kelele.
Uchaguzi ni mchakato mrefu lakini matokeo yake ni pande mbili, ama majuto ya miezi 60 au furaha kwa miezi kama hiyo kwa atakayeibuka mshindi tena akizidi hata kura moja tu.
Ama kweli, hiki ni chungu cha moto kilichobeba chakula jikoni, hapa mwenye kutumia maarifa atapata chakula kwa ajili yake na familia lakini mwenye kutumia nguvu pasi na maarifa atakipasua chungu na kumwaga chakula chini wakati mwenye hofu na woga atabaki kugugumia asijue cha kufanya hadi chakula kiunguwe.
Vyama vya siasa vitambue kuwa si wakati wa kusubiri nani afanye nini badala yake wekeni mashaka pembeni ili muanze kupelemba wapiga kura kwa kutoa elimu ya mpiga kura na umuhimu wa chaguzi hizi.
Kila mmoja atambue kilio kinamwenyewe, Habari ya kufanya mambo kwa kuiga na kutaka uwakilishwe ipo siku utajikuja hujui jambo lolote linalofanyika.
Nawapongeza CCM kwa kuamua kuanza na mbinu za kuipua chungu cha moto kikiwa salama, nawapongeza Chadema na wale walioungana kutafuta haki ya nani atasimamia uchaguzi huo. Wamefanya vema kutafuta haki mahali inakotafsiriwa badala ya kulia majukwaani, wanataka kushusha chungu kikiwa salama na chakula.
Najiuliza vyama vyenye usajili wa kudumu ambavyo viko kimya inaonyesha wazi wamekubali kushindwa hata kabla ya kushindana, huenda hawataki chakula au wametabiri kuwa chungu kimepoa.
Watanzania hawapendi kelele, tuache kulalamika hasa ikifika Novemba 28,2024 badala yake jipangeni kwani ng’ombe hawezi kunenepa siku ya mnada hata akatoa faida.
Tuviombe vyama vilivyojipanga kwa ajili ya uchaguzi viendelee kufanya hivyo kwa kufuata kalendo sahihi iliyotangazwa na wenye mamlaka lakini mwisho wa safari kila mmoja akubali matokea kwani kuna kushinda na kushindwa.
&&&&&&&&&&&&