Habel Chidawali- Dodoma
TATIZO la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa huenda ukapata ufumbuzi baada ya Wafamasia kutoka Jumuiya ya Madola kuanza kusambaza mafunzo ya kukabiliana na tatizo hilo.
Mafunzo hayo yanalenga kuwafundisha wafamasia mahospitalini kuwa na ujuzi wa kutengenza vitakasa mikono kupitia Jumuiya ya Madola ya wafamasia, kwa kushirikiana na Tropical Health and Education Trust (THET).
Akizungumza jana katika mafunzo hayo, mratibu wa mradi wa CwPAMS 2.0, Benard Makala alisema wanaendesha mafunzo ya kuzuia na kudhibiti maambukizi (IPC) kama sehemu ya kupambana na vimelea sugu vya magonjwa.
Makala ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma alisema mafunzo hayo yalianza mwaka jana katika Hospitali mbalimbali za Mikoa ya Dodoma, Katavi, Kilimanjaro na Mbeya ambako wamepata matokeo mazuri.
Akizungumza na watumishi na wafamasia wa Hospitali ya St Gemma Jijini Dodoma, Makala alisema kuwa kwa sasa kuna mzigo mkubwa wa maambukizi ya magonjwa yanayopatikana kwenye vituo vya afya na maeneo yanayotoa huduma za afya nchini.
“Tanzania ilikumbwa na maambukizi ya usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa yatokanayo vituo na ambapo inakadiriwa kuwa takribani vimelea milioni 1.29 vilitokea kwa mwaka 2020,” alisema Makala.
Mafunzo yanayotolewa yanajumuisha mazoea ya jumla ya IPC, na matumizi sahihi ya vitakasa mikono ili kuhakikisha mradi huu unadumu na unakua endelevu na kuwapatia malighafi na vifaa vya kutengenezea vitakasa mikono hospitalini hapo.
Kwa mujibu wa Makala, mafunzo hayo ni sehemu ya mradi mkubwa wa CwPAMS 2.0 ambao unatekelezwa kwa ushirikiano na Northumbria Healthcare ya Uingereza na Kilimanjaro Christian Medical Centre.
Hospitali tisa zilizonufaika na mpango hu oni Dodoma Christian Medical Center, Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi, Igawilo, Viwawa, Hospitali ya barali, na JKCI ya jijini Dar es Salaam kwa kufuata mpango wa Kudhibiti Usugu wa Dawa 2023-2028.
Mfamasia Mkuu katika Hospitali ya St Gemma Ambrose George alikiri kuwa mafunzo hayo licha ya kuwa ni ya muda mfupi, lakini yamekuwa msaada mkubwa kwani wahusika wanajifunza kwa vitendo moja kwa moja.
Ambrose alisema mbali na mafunzo ambayo wanapewa na taasisi hiyo,lakini walikabidhiwa malighafi za kutengeneza vitakasa mikono na kukabidhwa vifaa katika maeneo 10 ya muhimu katika hospitali hiyo.
Alisema wataendelea kuwafundisha na wataalamu wengine ambao hawakupata nafasi ya kujifunza hapo ili kupunguza tatizo la maambukizi ya vimelea kwa wafanyakazi wao na wagonjwa wanaopata huduma hapo.
Mwisho,…