KAMATI YA BUNGE YAMTAKA MKANDARASI AMALIZE UJENZI UWANJA WA NDEGE MIKUMI.
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imemtaka Mkandarasi anayejenga kiwanja cha ndege Kikoboga katika Hifadhi ya Taifa Mikumi kumaliza Kwa wakati.
Mkandarasi huyo Badr East Africa Enterprises Ltd anajenga uwanja huo kwa gharama ya Sh20.6 billioni lakini Ujenzi wake hauendi Kwa kasi inayotakiwa.
Ujenzi ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) na ulianza Mei 12, 2023 na unatakiwa kukamilika Desemba 10, 2024.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Timotheo Mnzava ameyasema hayo leo Septemba 9,2024 wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ya kukagua miradi ya REGROW kwenye hifadhi ya Taifa Mikumi, Mkoani Morogoro.
“Tunawapongeza kwa kazi nzuri iliyofanyika na inaonekana lakini msisitizo wetu ni muda. Mkandarasi amalize kazi kwa muda uliopangwa” amesisitiza Mhe. Mnzava.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii , Balozi, Dk. Pindi Chana yeye amesikitishwa na kitendo cha kuchelewa kwa mradi huo huku akimtaka mkandarasi kukamilisha kwa wakati la sivyo sheria itachukua mkondo wake kwani hakuna sababu ya maana katika ucheleweshaji huo.
Ziara hiyo ilimhusisha pia Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbasi na Watendaji na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Hifadhi ya Taifa Mikumi.
&&&&—-