Habel Chidawali-Dodoma
SERIKALI imeahidi kuwa itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuwalinda wananchi dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu wakiwemo tembo kwani ni wajibu wake kuhakikisha unakuwepo usalama wa wananchi.
Ahadi hiyo imetolewa leo Septemba 6, 2024 na Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Pindi Chana wakati akizungumza na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu kwenye kikao kilichofanyika ukumbi mdogo wa Pius Msekwa, Bungeni jijini Dodoma.
Waziri amesema umefika wakati wa kuwalinda wananchi na kuendelea kuchukua tahadhari za kutosha hasa kwenye maeneo ambayo ni korido za wanyamapori hivyo Taasisi zimeelekezwa kuweka vibao ili kuwataarifu wananchi wasipite katika maeneo hayo Chana.
Dk Chana amesema Wizara ya Maliasili na Utalii inatekeleza mikakati ya kukabiliana na wanyamapori wakali na
waharibifu kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanabaki salama lakini muhimu kuangalia namna ya kuwaelimisha wananchi ili wapande mazao ambayo hayavutii tembo kama ufuta, lakini wataalamu watawavalisha tembo viongozi kola za kuonyesha kundi la tembo linaelekea wapi na kujenga vituo vya askari wanyamapori.
Kwa upande wake Mbunge wa Meatu, Leah Komanya ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi nzuri ya uhifadhi na kupambana na changamoto ya tembo katika Wilaya ya Meatu kwa kuwapatia gari, pikipiki nne na kuwajengea kituo cha Askari Wanyamapori akisema vitasaidia kupunguza migogoro.
Awali, akiwasilisha taarifa ya Baraza la Madiwani, Diwani wa Kata ya Mwandoya, Basu Kayungilo amesema athari za wanyamapori wakali na waharibifu kwa wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyopakana na Pori la Akiba Maswa na Jumuiya ya Wanyamapori Makao zimekuwa ni za mara kwa mara.
Kayungilo amesema kuwa Baraza hilo liliazimia kuunda timu itakayoonana na Waziri wa Maliasili na Utalii ili kupata muafaka wa changamoto hiyo ikiwemo utaratibu wa malipo ya kifuta jasho/machozi na mgawanyo wa asilimia 25 zinazotolewa kama rufaa ya vijiji vinavyopakana na hifadhi.