Habel Chidawali-Dodoma
WAKRISTO duniani wamekumbushwa kukaa kwa Umoja na kusaidiana kama yanavyoelekeza maandiko katika Biblia na kufanya hivyo kutawasaidia katika kulinda Imani zao.
Wito huo umetolewa na Kasisi Kiongozi wa Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT) Canon Samwel Nyhinyinha wakati akifungua Mkutano wa waliokuwa Viongozi wa Idara ya Vijana wa Dayosisi hiyo ambao walikutana kwa nia ya kuunda umoja.
Mchungaji Canon Nyhinyinha amesema maandiko yanaelekeza watu kuishi kwa pamoja na kwa umoja lakini waweze kusaidiana kila mtu na mwingine ili kuzipata baraka zitokazo kwa Mungu mwenyewe.
“Zaburi ya 133 katika Biblia inasema ‘Tazama jinsi ilivyo vema na kupendekeza, Ndugu wakae Pamoja kwa Umoja’,na ninyi mmewaza jambo jema na kama mtalisimamia vema litakuwa na misingi mizuri ya kulisaidia Kanisa,” amesema Canon huyo.
Akizungumzia Umoja huo, ametaka viongozi hao kuwa na mipango itakayolisaidia Kanisa kusonga mbele na kutoa ushauri kwa viongozi wa idara ya vijana ambao wako madarakani kwa sasa ili wajifunze kupitia kwao.
Viongozi hao wa zamani wameahidi kuwa na mipango endelevu na kuwasaidia vijana walioko madarakani ili watimize ndoto zao na kulifanya Kanisa hasa kwenye idara ya vijana kuwe na maendeleo.
Kwenye Mkutano huo Mwenyekiti wa zamani wa idara ya Vijana wa Dayosisi Justin Chidawali alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa viongozi wa zamani huku Aman Mganga akichukua nafasi ya Katibu na Emmy Jacobo kuwa Mtunza Fedha.
Akiahirisha Mkutano huo, Mwenyekiti Justin aliwataka viongozi wa zamani kuzingatia misingi ya kiutumishi na kutambua kuwa wapo viongozi walioko madarakani ambao kwa namna yoyote wanapaswa kuheshimiwa na kusaidiwa inapobidi ili idara ya vijana iwe na mchango mkubwa ndani ya Dayosisi.
“Dayosisi yetu ni kubwa, wako viongozi wa vijana na idara zingine walioko madarakani hao lazima tuwaheshimu na kutambua majukumu yao, tuwasaidie ili wafikie ndoto zao ndipo nasi Umoja wetu utasimama na kuwa na nguvu,” alisema Justin.
Katibu wa Umoja huo Aman Mganga ametaja malengo ya kuanzishwa kwa Umoja huo ni kusaidiana kwenye shida na raha pamoja na kujengeana uwezo kiuchumi kwa kila mtu atakapotumia fursa ya mwingine.
$$$$$$$ $$$$$$$$$$$$$