Habel Chidawali-Dodoma
WIZARA ya Katiba na Sheria katika kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imewafikia wananchi zaidi ya 490,000 katika mikoa saba nchini huku ikiahidi kuendelea kutoa huduma hiyo zaidi.
Lengo ni kuhakikisha kuwa huduma za msaada wa kisheria zinapatikana kwa wananchi katika maeneo yote ili wasioweza kuifikia haki kwa kukosa huduma za mawakili waweze kuifikia kwa urahisi kupitia huduma za msaada wa huduma za kisheria.
Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Msaada wa Huduma za Kisheria Ester Msambazi anasema Wizara ya Katiba na Sheria imejipanga kuhakikisha hakuna mtu anakosa huduma za kisheria katika kipindi hasa kwenye Kampeni ya Mama Samia.
Msambazi ambaye ni Msajili wa Mashirika yanayotoa Msaada wa Huduma za Kisheria amesema kampeni hiyo inatekelezwa katika ngazi ya jamii kwa kutumia majukwaa na maonyesho mbalimbali ili kuwafikia wananchi wengi.
Akizungumzia maonyesho ya nanenane amesema kikosi chao kimejipanga kutoa huduma mbalimbali ikiwemo ushauri kwa wanandoa, mirathi,matunzo ya Watoto na migogoro mingine na masuala ya migogoro hivyo akaomba wananchi kujitokeza kupata huduma hizo ambazo ni bure.
“Huduma zingine tunazozitoa ni kuwaandalia wananchi nyaraka za kuwasilisha mahakamani na kutoa elimu kwa makundi ikiwemo wanafunzi na wamama wa vikoba na tunasikiliza migogoro ya mtu mmoja mmoja kwani hadi sasa tumeshasikiliza zaidi ya watu 23,” amesema Msambazi.
Amesisitiza kwa wananchi walio nje ya Jiji la Dodoma ambao hawawezi kufika kwenye maonyesho, wameshauriwa kufika kwenye ofisi mbalimbali zinazotoa misaada ya kisheria ili waweze kuhudumiwa.
Balagumu Media, Sauti ya Mnyonge