Habel Chidawali-Dodoma
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza mkakati wa kumaliza matatizo ya wafanyabiashara walipakodi ili waone umuhimu wa kulipa kodi kwa hiyari bila kusukumwa.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishina wa TRA Yusuph Mwenda wakati akizungumza na waandishi wa Habari na wananchi waliojitokeza katika banda lao kwenye Maonyesho ya Wakulima viwanja vya Nanenane Nzuguni.
Kamishina Mwenda amesema Mamlaka hiyo inakuja kivingine ili kuondoa malalamiko ambayo yamekuwepo kwa wafanyabiashara na kwamba mkakati wao ni kuja kivingine baada ya kelele hizo.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na mvutano kuhusu wafanyabiashara na Mamlaka hiyo katika mvutano ulioanzia soko la Kariakoo Jijini Dar es Salaam na baadae kuibukia mikoa mingine ingawa hakukuwa na joto kubwa.
“Tumejipanga sana kumaliza matatizo ya walipakodi,hili ni mojawapo ya maeneo tunayochukua changamoto za walipa kodi na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka, nitoe wito waje, waonena na watu wetu, waeleze changamoto zao,” amesema Mwenda.
Kwa mujibu wa Kamishina huyo, TRA imejipanga kuwahudumia walipakodi kwa haraka na kurahisisha biashara zao ili waweze kulipa kodi na kuchangia maendeleo ya Taifa huku akisisitiza ulipaji kodi unapaswa kuwa rafiki.
Amesisitiza kwa Wafanyabiashara kutoa risiti wanapouza bidhaa zao lakini muhimu wa wananchi nao kudai risiti kila wanunuapo bidhaa mbalimbali.
Akizungumzia maonyesho ya wakulima, amesema kilimo ni biashara hivyo lazima Mamlaka hiyo ishiriki na kuendelea kutoa elimu lakini akaagiza watumishi walioko kwenye mabanda ya TRA kuendelea kutoa elimu ya mlipa kodi.
Balagumu Media, Sauti ya Mnyonge