KISA HUDUMA NZURI,ANUNULIWA KIWANJA NA WANANCHI
Na _Bernadetha Mwakilabi, Kongwa_
Wananchi wa kijiji cha Ngomai Kata ya Ngomai wilayani Kongwa wamefanya harambee ya kumpongeza Muuguzi wa kijiji chao Peter Mwakalosi wakidai ni mwajibikaji kwenye huduma na upendo mkubwa kwa wagonjwa wake.
Mapema wiki hii wananchi katika Kijiji hicho waliamua kuchangishana kwa hiyari na kupata zaidi ya Sh4 milioni ambazo walizitumia kumnunulia kiwanja Muuguzi huyo ili ajenga na kuishi kijijini hapo hata atakapostaafu utumishi wake.
Katika risala yao iliyosomwa kwa Mkurugenzi wa Wilaya hiyo Dk Omary Nkullo wananchi hao walipongeza kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan lakini miongoni mwao ni kuwa na watumishi wenye kuwajibika na kujali utu wa watu kama ilivyo kwa Muuguzi huyo ambaye amekuwa mstari wa mbele kusaidia watu wa kijiji hicho na vijiji jirani.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Kongwa Dk Omary Nkullo amewapongeza wananchi wa Ngomai kwa kuandaa harambee hiyo akisema wameonesha moyo wa shukrani na jambo la kuigwa kwa watu wengine na kuongeza kuwa hilo ni deni ambalo anatakiwa kulipa muuguzi huyo.
Dk Nkullo amefafanua kuwa harambee iliyofanywa na wananchi hao imeonesha kuwa Mwakalosi anatambua nafasi yake katika utendaji wa kazi na hii inatokana na kazi kubwa anayoifanya chini ua Serikali ya Rais Samia ya kulipa watumishi kwa wakati na kuboresha miundombinu ya afya nchini.
Diwani wa kata ya Ngomai Mfalme Mlimila amemuomba Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kongwa kutokumhamisha Muuguzi huyo kijijini hapo kwani anafanya kazi nzuri ya kutoa huduma nzuri ya afya na wananchi wanamkubali.
Mlimila amesema Muuguzi huyo alipofika kijijini kwao mwaka 2005 amefanikiwa kuondoa dhana potofu ya wananchi kutibiwa kwa waganga wa kienyeji magonjwa ambayo awali hawakuamini kama yanaweza kutibiwa hospitalini na kupona.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya ya Kongwa Dk Thomas Mchomvu amesema zahanati ya Kijiji Cha Ngomai huzalisha Watoto kati ya 30 hadi 40 kwa mwezi huku wilaya ikiwa na takwimu za kuzalisha watoto 1300 hadi 1400.