ASA yashusha aina tatu mpya za mbegu ili kuongeza uzalishaji,
Na Habel Chidawali
Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) imeingiza nchini aina tatu mpya za mbegu ya alizeti, ngano na mtama ili kuongeza uzalishaji kwa wakulima wa ndani na sekta hiyo kwa ujumla wake.
Hata hivyo, wilaya 12 zimenufaika moja kwa moja kwa kupelekewa mbegu katikamaeneo yao hivyo wakulima wanaitwa kuzichukua kwa ajili ya msimu wa Kilimo unapoanza.
Katika taarifa aliyotoa akiwa kwenye banda la maonyesho ya Wakulima Nzuguni, Kaimu Meneja wa ASA Benjamin Mfupe, amezitaja mbegu hizo kuwa ni TARISO II (Mtama), Sun Bloom (alizeti) na SST 884 ya ngano ambapo zimeingizwa nchini ili kukidhi azma ya sasa ya mahitaji makubwa ya mbegu bora ndani ya sekta hiyo.
“Hadi sasa tumeshaagiza kutoka nje angalau tani 700 za aina ya Sun Bloom, mbegu nzuri ambayo inawawezesha wakulima kupata mavuno kati ya gunia 16 hadi 18 kwa ekari moja na kusema mbegu hiyo inauzwa kwa Sh0,000 kwa kilo moja, badala ya Sh45,000 kama inavyouzwa na makampuni mengine ya mbegu,”amesema Mfupe.
Amesema kwa kuzingatia uwezo wa kukua wa aina hiyo, wakulima watapata nafasi ya kuvuna alizeti takribani siku 110 baada ya kupanda tena mbegu hiyo husaidia kwa wingi wa mavuno kutokana na aina yake ya kukomaa ambapo hutoa kichwa kikubwa chenye mbegu bora ya mafuta.
Kwa upande wa ngano amesema ni zamu ya wakulima wa zao hilo kuonyesha tabasamu kwa madai kuwa aina mpya ya SST 884 inayoagizwa kutoka nje ina uwezo wa kukua na kustahimili aina mbalimbali za udongo na magonjwa yenyewe ikichukua kati ya siku 90 hadi 110 kwa wakulima kuvuna na ekari moja inaweza kuzalisha gunia 14 na 18.
Amezitaja Wilaya 12 zilizonufaika na mpango huo ni Makete, Makambaku, Njombe, Arusha, Wangin’gombe, Ludewa, Siha, Monduli, Hanang, Babati, Sumbawanga, na Nkasi na tayari ASA imeshasambaza jumla ya tani 692.9 za ngano iliyotengenezwa kienyeji lakini zimeboreshwa na kufaa kwa matumizi ya mbegu.
Kuhusu mtama aina ya TARISO II, Mfupe amesema mbegu hiyo imeagwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), na kuwa ina uwezo wa kustahimili magonjwa, wakiwemo ndege waharibifu lakini inaweza kutoa kati ya gunia 14 na 16 kwa ekari moja.
&&&&&&&&&&&&